.

.

13 Mei 2015

WILAYA YA MBEYA MJINI YAONGOZA KWA MATOKEO BORA YA KUJIFUNZA

images modified
13 Mei 2015, Dar es Salaam: Watoto wa Afrika Mashariki hawajifunzi stadi za msingi za kusoma na kuhesabu. Ni watoto wawili tu kati ya kumi (20%) wa darasa la tatu wanaoweza kusoma na kufanya hesabu za darasa la pili. Wanapohtimu elimu ya msingi, mtoto mmoja kati ya wanne Afrika Mashariki (24%) anakuwa bado hajamudu stadi za kusoma na kuhesabu.
Matokeo haya yametolewa na Uwezo iliyopo Twaweza, kwenye ripoti yao Je, Watoto wetu wanajifunza? Uwezo wa kusoma na kuhesabu Afrika Mashariki. Takwimu za matokeo ya kujifunza, hali ya shule na kaya zilikusanywa mwaka 2013. Zilijumuisha wilaya zote Afrika Mashariki kupitia tathmini ya kaya iliyofanywa na wananchi wenyewe. Matokeo ya kujifunza hutathminiwa kwa watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 16 kupitia majaribio yaliyotungwa kwa mtaala wa ngazi ya darasa la pili.

Asilimia 64 ya watoto Kenya walifaulu majaribio yote ya kusoma na kuhesabu. Nchini Tanzania ni asilimia 48 na Uganda asilimia 36 tu waliofaulu majaribio yote. Hii ina maana kwamba, hata Kenya, nchi inayofanya vizuri kuliko zote Afrika Mashariki, ina watoto asilimia 36 wasiozimudu stadi za msingi za kusoma na kuhesabu katika ngazi ya darasa la pili.
Wilaya ya Mbeya Mjini imeibuka kuwa wilaya yenye ufaulu wa juu kabisa Afrika Mashariki. Hata hivyo, wilaya nyingine kumi zenye ufaulu wa juu zimetoka nchini Kenya. Wilaya za Tanzania mara nyingi hupata ufaulu wa kati wakati Uganda imekuwa ilishika nafasi ya chini kabisa. Wilaya iliyofanya vizuri zaidi nchini Uganda ilishika nafasi ya 82 kati ya wilaya zote za Afrika Mashariki.
Kipato cha familia kimeonekana kuwa na uhusiano na matokeo ya kujifunza: lipo pengo kubwa kati ya maskini na wasio maskini
Asilimia 70 ya watoto nchini Kenya waliotoka kaya zisizo maskini walifaulu jaribio moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia 44 tu ya watoto waliotoka kaya maskini sana waliokuwa na uwezo huo huo.Asilimia 55 ya watoto nchini Tanzania waliotoka kaya zisizo maskini waliofaulu jaribio moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia 39 tu ya watoto waliotoka kaya maskini sana waliokuwa na uwezo huo huo.Asilimia 42 ya watoto nchini Uganda waliotoka kaya zisizo maskini waliofaulu jaribio moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia 24 tu ya watotowaliotoka kaya maskini sana waliokuwa na uwezo huo huo.
Licha ya tofauti zilizopo nchini Kenya, kaya maskini zaidi nchini humo, bado zinafanya vizuri kuliko kaya zisizo maskini za Uganda.
Cha kusikitisha ni kuwa hakuna mabadiliko makubwa kwenye matokeo ya kujifunza kwa kipindi cha miaka minne iliyopita (2010 hadi 2013). Licha ya uandikishaji umebaki kuwa juu tangu kuanzishwa kwa elimu ya bure ya msingi kwa wote katika nchi zote tatu.
Vipimo vya Uwezo hutumiwa kutathmini mwenendo wa utekelezaji wa Malengo ya Elimu kwa Wote. Malengo haya yaliahidiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka 15 kuanzia 2000 hadi 2015 na yalilenga kuinua ubora wa elimu. Kwa ujumla, hakuna mabadiliko makubwa kwenye kiashiria chochote kilichotumika kutathmini malengo haya ndani kipindi cha miaka minne iliyopita. Hata hivyo, uandikishaji umebaki kuwa juu katika nchi zote tatu zikiwa na wastani wa uandikishaji wa 90%. Vile vile usawa wa kijinsia umefikiwa katika nchi zote tatu kwenye nyanja za uandikishaji na ubora. Hakuna tofauti iliyobainika kwenye fursa ya kuandikishwa kati ya wavulana na wasichana. Lakini, usawa huo huo upo pia kati ya wavulana na wasichana katika kufanya vibaya kwenye matokeo ya kujifunza.
Dk. John Mugo, Mkurugenzi wa Utafiti wa Twaweza alisema "tofauti kubwa baina ya nchi na baina ya wilaya, zinaonesha kuwa Afrika Mashariki itaendelea kugawanyika zaidi. Aidha, utafiti huu unaonyesha kwamba matokeo hayajabadlika miaka yote hii. Hii hi ishara tosha kwamba hatujatilia mkazo umuhimu wa watoto wote kujifunza wakiwa shuleni"
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, aliongeza "Mafanikio yaliyofikiwa katika kuongeza fursa za kujiunga na shule na usawa wa kijinsia yanapaswa kupongezwa. Lakini takwimu hazifichi ukweli kwamba wananfunzi wengi mno baado hawajifunzi. Tusilegeze uzi katika uandikishaji wa watoto. Jambo la msingi zaidi ni kuhakikisha kwamba watoto wote wananjifunza stadi zote za msingi – kusoma na kuhesabu."
Uwezo ilitathmini watoto zaidi ya 325,000 wenye umri kati ya miaka 6-16 katika takriban kaya 150,000. Hii ilijumuisha wilaya 366 nchini za Kenya, Tanzania na Uganda. Pia ilikusanya takwimu kutoka shule za msingi za serikali zaidi ya 10,000.
Ripoti hii, ikiwa pamoja na mifano ya majaribio yaliyotumika, vinapatikana hapa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni