.

.

29 Juni 2015

NCHI INAPOJIANGALIA KWENYE KIOO CHA CCM

Ndugu zangu,
Jana jioni pale Viwanja vya Furahisha Mwanza, tulionyeshwa kupitia runinga, CCM ikiongozwa na Katibu wake Mkuu, Abdulhaman Kinana ikifanya mkutano wa hadhara.
Ni tukio la kuhitimisha ziara za kutembea nchi nzima ikiwamo wilaya, kata na vijiji iliyofanywa na Abdulhaman Kinana na timu yake. Kuna niliyokuwa nikiyatafakari wakati nikiangalia.
Nakiona Chama Cha Mapinduzi kama kioo ambacho nchi nzima ndio inachokichukua kujitazamia. Hata walio kwenye upinzani na CCM wanajitazama kupitia kioo cha CCM. Si ajabu kabisa kuona hata walio kwenye upinzani wanatoa maoni juu ya watangaza nia ya Urais kupitia CCM. Kwamba utasikia inasemwa kutoka kwa wapinzani; kuwa fulani hafai, afadhali ya yule, ndani ya CCM!
Ingawa kuna haja pia ya walio kwenye upinzani kutengeneza vioo vya kujitazamia, lakini, hakuna ajabu ya wapinzania kujitazama kupitia kioo cha CCM. Kiukweli CCM kuanzia TANU, si tu imekuwa madarakani muda wote, lakini, ndio Chama kilichojenga misingi ya nchi hii. Hakuna ajabu basi, kuwa hata ninapoandika fikra hizi. Vyama vya upinzani vinaisubiri CCM kwanza itangaze mgombea wake Urais ndivyo navyo vifuatie.
Kimsingi, CCM ni zaidi ya Chama cha Siasa. Ni taasisi kubwa na inayoongoza kwenye nchi. CCM imebeba maslahi ya kina na mapana ya Watanzania zaidi ya milioni 44. Katika hali tuliyo nayo sasa, CCM haipaswi hata kidogo, kufanya maamuzi ya ovyo na ya kijinga yatakayoigharimu nchi hasara ya miaka mingi.(P.T)
Katika wakati tulio nao sasa, kama chama cha siasa kitataka kibaki kwenye mamlaka ya uongozi kwa muda mrefu , na kwa kupitia masanduku ya kura, basi, kina lazima ya kutafuta kuungwa mkono wa walio wengi kwa maana ya watu.
Mwanafalsafa Benjamin Disrael anasema;
“ Mamlaka zote msingi wake ni imani, tunawajibika katika kuyatekeleza yaliyo kwenye mamlaka zetu, na kwamba, mamlaka yatatokana na watu, kwa ajili ya watu, na chemchem zote za fikra ziachwe hai”- Benjamin Disraeli.
Kwa kukiangalia anachosema Disraeli tunaona, kuwa kazi ya Chama ya cha siasa haipaswi kuwa ni kuudhibiti umma katika kuhoji yanayofanywa na Serikali, badala yake, Chama kinapaswa kuwa upande wa umma. Ni katika kuyaelewa mahitaji ya umma.
Na kwa vile Serikali inapaswa kuwa mtekelezaji wa yale yaliyoamuliwa kwa niaba ya umma, basi, kazi kubwa ya chama cha siasa ni kuisimamia Serikali katika kuutekeleza wajibu wake huo. Na hapa tunaona ni moja ya kazi iliyofanywa vema na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana na timu yake. Kinana hakujitanguliza yeye, alikitanguliza Chama kama nyenzo ya kuwatetea wananchi kwa kuibana Serikali. Kinana na wenzake wamefanya kazi ya kufuta vumbi la kwenye kioo cha CCM.
Ikumbukwe pia, katika nchi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi huimarika zaidi kwa kuwepo na uhuru wa kifikra. Kwamba uwepo wa tofauti za kifikra si jambo baya, bali ni jema na la muhimu kwa maendeleo ya nchi, kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kwamba siku zote, mawazo na mahitaji ya wananchi yatangulizwe.
Hivyo basi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi huchangiwa pia na uwepo wa wananchi wenye uwezo wa kutathmini michango itokanayo na wengine katika jamii husika.
Ni muhimu pia kukawepo kwa wanasiasa wenye uwezo wa kutathmini mambo na kuja na hoja zenye mashiko kwa maslahi ya nchi, badala ya hoja zenye kulenga kuibakisha nchi kwenye hali ya kugota kisiasa na kimaendeleo ya kiuchumi.
Nasisitiza hapa, uwepo wa siasa za vyama vingi ni jambo jema kwa nchi, lakini, kukosekana kwa umakini katika kuendesha siasa za vyama vingi hupelekea kupunguza ladha na maana ya kuwa na siasa za vyama vingi. Maana, vyama vingi ina maana pia ya uwepo wa fikra nyingi zenye kutofautiana na hata kufanana, lakini, ni vema zikawa ni zenye kujenga na kulinda maslahi ya nchi.
Na hapa tulipo, CCM imekuwa ndio kioo cha nchi kujitazamia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni