Kocha Mkuu wa Mbeya City Fc, Kinnah Phiri ametangaza majina ya nyota 18
watakaoivaa Simba Sports Club kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania
bara uliopangwa kuchezwa jumapili hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Mapema leo Phiri ameuambia mtandao huu kuwa anatua jijini Dar na kikosi
cha nyota hao ambao aliwaandaa maalumu kwa mchezo huo wa mwishoni mwa juma
akiwa na imani kubwa kuwa wataiwezesha City kuibuka na ushindi kutokana na
‘kuiva’ vizuri kimazoezi na mafunzo waliyoyapata katika wiki nzima ya
maandalizi kupitia mifumo mbalimbali aliyokuwa akiifundisha .
“Nina imani nao,wamefanya vizuri sana kwenye mazoezi ya wiki hii, sina
shaka na wao kutupatia matokeo kwa sababu wako sawa tayari kwa mchezo,tutacheza
kwenye mfumo mpya ambao haujawahi kuonekana tukicheza, hii ni kwa sababu
tumedhamiria kupata ushindi kama ambavyo timu imekuwa ikifanya kila inapokutana
na Simba”, alisema.
Miongoni mwa nyota walio kwenye orodha ya kuivaa Simba siku hiyo ya
jumapili ni pamoja na beki wa kushotoHassan Mwasapili, mlinda lango Haningtony
Kalyesubula pia wamo Temi Felix, Haruna Shamte,Yohana Moriss,Kenny
Ally,Geoffrey Mlawa,Issa Nelson na wakali wengine 10 ambao wamepewa majukumu
kadhaa kuhakikisha City inaandikisha pointi tatu muhimu mbele ya timu hiyo ya
Msimbazi.
Huu utakuwa ni mchezo wa sita kwa timu hizi kukutana katika michuano
hii ya ligi kuu ya vodacom huku City ikifanikiwa kushinda mara mara mbili sare
mbili na Simba ikishinda mara moja katika michezo mitano iliyozikatanisha timu
hizi hapo awali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni