STRAIKA wa Prisons, Jeremiah Juma ameweka wazi kuwa hana papara
ya kuondoka ndani ya kikosi hicho kwani hakuna timu inayoweza kununua
ajira yake kwa sasa ingawa kuna timu zinamnyemelea.
Jeremiah
ambaye pia aliitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa
mara ya kwanza kilichokuwa kinajiandaa na mechi dhidi ya Chad ya kuwania
kufuzu fainali za Afcon aliliambia Mwanaspoti kuwa anaamini umri wake
bado unamruhusu kusubiri na kuendelea kuwemo kwenye kikosi cha Maafande
hao hivyo kwa msimu huu hajafikiria kuondoka.
Alisema
kuwa endapo ataondoka kwenda timu nyingine ambayo si ya kijeshi basi
wawe wamemuandalia kitita cha maana ambacho kitamshawishi kuacha ajira
hiyo ambayo ameitumikia kwa mwaka mmoja kati ya mkataba wa miaka mitatu.
“Si
kwamba hakuna timu ambazo zimeonyesha nia, zipo nyingi tu ila siwezi
kuzikubalia kutokana na dau ambalo huwa wananiambia, ni dau dogo sana
ambalo haliendani na thamani ya ajira yangu, hivyo siwezi kuacha ajira
na kukimbilia fedha ya msimu ambayo ni ndogo mno, muda ukifika na kwa
fedha ya maana nitaweza kuondoka.
“Mkataba wangu ni
kwamba siku nikiamua kuacha ajira basi na mkataba wa timu utakuwa
umemalizika hapo yanakuwa ni makubaliano yangu na wanaonihitaji, ila
kwasasa acha niendelee kuwepo hapa nikijijenga zaidi, ila nawashauri tu
wachezaji kuwa kipindi hiki cha usajili wawe watulivu na wasikurupuke
kutoa uamuzi,” alisema Jeremiah ambaye amefunga mabao 12 mpaka sasa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni