Wakati
sakata la kampuni ya Lugumi Enterprises likiendelea kutikisa nchi,
mashine za utambuzi wa alama za vidole, zimeanza kufungwa katika mikoa
kadhaa ikiwamo ya Dodoma na Geita.
Uchunguzi
wa Mwananchi unaonyesha kwamba juzi mashine hizo zilifungwa katika
vituo vya polisi vya wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma na kazi
hiyo ilitarajiwa kufanywa mjini Dodoma jana. Pia, vyanzo vya habari
kutoka mkoani Geita vimeithibitishia Mwananchi kwamba mashine hizo
zimefungwa katika vituo vitano vya polisi.
Kampuni
ya Lugumi iliingia mkataba na Jeshi la Polisi mwaka 2011 kufunga
mashine hizo kwenye vituo 108, lakini hadi wakati Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anamaliza ukaguzi, ni vituo 14 tu
vilikuwa vimefungwa mashine hizo.
Taarifa
hiyo ya CAG ililistua Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
iliunda kamati ndogo ili kuzunguka mikoani kuthibitisha taarifa hiyo ya
mkaguzi mkuu.
Lakini wakati kamati hiyo ikiwa imepewa kazi hiyo, Mwananchi imeambiwa kuwa mashine hizo zinafungwa.
“Tulikuwa na Lugumi hapa,” alisema mmoja wa watoa habari waliozungumza na Mwananchi.
“Vijana wa Lugumi walikuwa wanafunga mashine, wameondoka kwenda Kongwa. Kesho (jana) watakuwa Dodoma.”
Imeelezwa
kuwa vijana wanaofunga mashine hizo walikwenda Mpwapwa wakitokea Kibaha
mkoani Pwani. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, katika Mkoa wa Geita,
mashine hizo zimefungwa wilaya za Nyang’hwale, Chato, Geita, Bukombe na
Mbogwe.
Alipotafutwa
kutoa ufafanuzi wa kazi ya ufungaji mashine hizo, Kamanda wa Polisi
mkoani Geita, Latson Mponjoli alisema suala hilo ni la kitaifa hivyo
kutaka watafutwe viongozi wa kitaifa.
“Mimi
nitazungumzia nini kuhusiana na Lugumi? Suala hilo ni la kitaifa
unaniuliza mimi? Hilo suala mtafute waziri mwenye dhamana au IGP
(Inspekta Jenerali wa Polisi) ndiyo wenye mamlaka ya kulizungumzia jambo
hilo,” alisema Kamanda Mponjoli.
Lakini
juhudi za kumpata IGP Ernest Mangu kwa simu hazikufanikiwa badala yake
simu yake ilipokewa na msaidizi wake. Mwandishi alipoanza kuzungumza
naye, simu yake ilikatika.
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hataki kujibu maswali
yanayohusu kampuni hiyo na kwamba mwandishi awasiliane na kampuni hiyo.
“Taarifa za Lugumi kawaulizeni Lugumi wenyewe, sipendi kujibu maswali ya
kijinga na upumbavu, kwa sababu nimekwenda vituoni mwenyewe
nimejionea,” alisema na kukata simu. Alipopigiwa simu tena ili aeleze
amejionea nini hakupokea.
Hata
hivyo, hakuna mtu yeyote kutoka Lugumi ambaye amekuwa tayari kuzungumza
ingawa vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vimesema
kwamba utekelezaji wa kazi ya kufunga kompyuta hizo aina ya Dell
umeanza.
“Unajua
hili ni agizo na amri ya kamishna mmoja wa makao makuu. Kuna gari
lililofuata vifaa hivyo makao makuu na kompyuta hizi zilifika hapa
Jumatano na zikafungwa Alhamisi, lakini kama nilivyosema haziwaki na
hata askari hawana mafunzo ya kuzitumia,” alisema mpashaji mwingine
aliyeomba jina lake lihifadhiwe.
Mtoa
taarifa huyo alisema uharaka wa kufunga mashine hizo unafanywa ili
kujiandaa kwa ukaguzi wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) wanaotarajiwa kupita wilayani na mikoani kuthibitisha
uwepo wa mashine hizo. Kwamba watakapofika wakaguzi wadhani kwamba vifaa
hivyo vilikuwapo tangu awali wakati si kweli.
‘’Ndugu
yangu, huwezi kuamini kompyuta za Lugumi zimewasili hapa mkoani kwetu
(Geita), lakini sasa zimeletwa kwa lengo moja tu kuwahadaa wakaguzi
kwamba zilikuwepo tangu awali wakati si kweli. Hizo kompyuta zililetwa
Jumatano wiki iliyopita na zilifungwa Alhamisi na mbaya zaidi haziwaki,
yaani ni mbovu,” alisema mtu huyo.
Mjumbe
mmoja wa PAC aliwahi kulalamika kuwa kuna mchezo unachezwa wa
kukwamisha kamati ndogo baada ya Bunge kuchelewa kutoa fedha za
kuwezesha kazi ya ukaguzi kuanza kwa lengo la kutoa mwanya wa kufungwa
kwa mashine hizo nje ya muda.
Juhudi
za kumpata Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillaly ili atoe ufafanuzi
wa kazi hiyo kufanywa sasa tena na polisi wenyewe, hazikuzaa matunda.
Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, ambaye ni mwenyekiti wa kamati
ndogo ya PAC iliyopewa jukumu la kuchunguza sakata la Lugumi kwa siku
30, alisema mambo yote yatakuwa kwenye ripoti yao. “Kama wanafunga
mashine au hawafungi hilo sijui, we subiri tu tumalize kazi tutatoa
ripoti,” alisema.
Habari zinasema tayari kamati hiyo iliyogawanywa katika makundi matatu imekamilisha ukaguzi katika Mkoa wa Dodoma.
Kamati
ya PAC ndiyo iliyoibua sakata hilo katika vikao vya kamati vya Aprili,
ikinukuu ripoti ya CAG ya mwaka 2014/2015 kwamba kampuni hiyo iliyoingia
mkataba na Polisi kufunga mashine hizo haikuwa imekamilisha kazi hiyo.
Pamoja
na kutokamilisha ufungaji mashine hizo, Lugumi ilishalipwa Sh34 bilioni
sawa na zaidi ya asilimia 90 ya jumla ya malipo ya Sh37 bilioni za
mkataba, jambo ambalo wabunge wanaona ni viashiria vya ufisadi katika
Jeshi la Polisi.
Katika
sakata hilo, pia anatajwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
akitakiwa ajiuzulu kwa madai kuwa ana hisa kwenye kampuni ya Infosys,
ambayo ilitoa ushauri wa kitaalamu kwenye mradi huo, ikiwa imeombwa na
kampuni ya Kimarekani ya Biometrica ambayo iliipa Dola 75,240 (sawa na
zaidi ya S150 milioni).
Hata
hivyo, Infosys imenukuliwa ikidai kuwa Kitwanga alishajiondoa kwenye
uendeshaji wa kampuni hiyo mwaka 2010 na tangu wakati huo hajakanyaga
kwenye ofisi zao.
CHANZO: MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni