JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE.
UMMY MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO KUHUSU WANANCHI KUSHAMBULIA WATUMISHI WA AFYA HASA MADAKTARI NA
WAUGUZI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI, TAREHE 29 MACHI, 2016
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa
hii nikiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya nchini, kutoa tamko
kuhusiana na matukio ya hivi karibuni yaliyoripotiwa kwenye vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kuhusiana na vitendo vya kusikitisha
wanavyofanyiwa watumishi wa sekta ya afya, wakiwemo Madaktari kama vile
kushambuliwa kwa maneno na vipigo. Pasi na shaka, vitendo hivyo
vitaathiri upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wanaopewa
huduma hizo hususan wa kipato cha chini.
Matukio haya
yanajumuisha tukio lililotokea tarehe 27.03.2016 katika Hospitali ya
Mkoa wa Mtwara, Ligula, ambapo Dr Dickson Sahini alishambuliwa na ndugu
wa mgonjwa aliyepelekwa hapo kuhudumiwa.
Napenda kutamka
kwamba nimesikitishwa sana na tukio hilo, na ninalaani vikali matukio ya
watumishi wa afya kushambuliwa kwa maneno au kwa vitendo na wananchi
wanaopatiwa huduma. Jambo hili likiendelea litawavunja moyo watumishi wa
afya na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ningependa
kuwafahamisha kwamba kwa ujumla wake sekta ya afya inakabiliwa na
changamoto nyingi sana katika maeneo ya miundombinu, dawa na vifaa tiba,
watumishi wa kutosha, pamoja na kuwa na watumishi wasiozingatia
nidhamu, weledi na maadili katika kutimiza majukumu yao.
Ninatambua
kwamba changamoto hizi zipo siku nyingi, na zimekuwa zikitafutiwa
majawabu na Serikali za awamu zilizopita ikiwemo ile ya awamu ya nne.
Lakini sote ni mashahidi kwamba Serikali ya awamu ya tano, chini ya
uongozi wa Mheshimiwa Dr John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, inachukua hatua za makusudi katika kutatua
changamoto hizi, likiwemo pia suala zima la utendaji unaozingatia
uwajibikaji.
Kwa hiyo
ninawasihi sana wanachi wanaopatiwa huduma katika vituo vyetu vya afya
kote nchini kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi na
kufanya vitendo vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya. Kwa vile nchi
yetu inafuata misingi ya utawala unaozingatia sheria, ni vyema wananchi
wakafuata taratibu zilizowekwa wanapohisi kwamba hawakupatiwa huduma za
afya wanavyostahili.
Aidha nachukua
fursa hii kuvitaka vyombo na mamlaka husika kutosita kuwachukulia hatua
wananchi wanaokwenda kinyume na matakwa ya sharia ili kuwahakikishia
watoa huduma za afya usalama na amani wakati wa utoaji wa huduma hiyo.
Ninaagiza vile
vile kwamba hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini
ziweke utaratibu mwepesi wa wananchi kufikisha malalamiko yao pindi
wanapoona kwamba hawakupatiwa huduma za afya kwa kiwango stahiki.
Napenda pia
kuahidi kwamba tutajitahidi kutatua changamoto za kimfumo zilizopo
katika utoaji wa huduma za afya nchini ili kuufanya utoaji wa huduma
kuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Ninatambua
kwamba sehemu kubwa ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanafanya
kazi zao kwa ufanisi, upendo, uadilifu na kwa kuzingatia matakwa ya
weledi (professionalism) na miiko ya taaluma zao (ethics). Pia
ninatambua kwamba wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na
wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona
wapo salama. Ninawapongeza kwa dhati watumishi hawa na ninawashukuru na
kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri, kwa maslahi ya Taifa
letu.
Hata hivyo
ninasikitishwa sana na tabia ya watumishi wa afya wachache ambao
wanafanya kazi kinyume na maadili na matakwa ya weledi wa taaluma zao.
Napenda kusisitiza kuwa Wizara yangu haitavumilia matukio ambayo
watumishi wa Sekta ya Afya watakwenda kinyume na matakwa ya weledi na
maadili ya taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hivyo hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.
Nimeshaelekeza
vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani
Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga
Tanzania (TNMC) kuchukua hatua mara moja, kwa mujibu wa Sheria na
Taratibu zao, juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa kukiuka misingi ya
weledi na maadili ya taaluma zao. Endapo tuhuma zao zitathibitika, hatua
stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao
ikibidi.
Hivyo kwa tamko
hili ninawaasa na kuwaagiza watoa huduma wa afya wote nchini kufanya
kazi zao kwa bidii, kwa nidhamu na kwa kuzingatia weledi na maadili ya
kitaaluma kama inavyoelekezwa.
Ndugu Wananchi,
Napenda pia
kukumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa mahusiano mema kati ya watoa
huduma za afya na wananchi, na usimamizi wa weledi na maadili katika
vituo vya kazi, itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa Mikoa
na Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Kamati za Usimamiaji wa Huduma
za Afya za Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamiaji wa Huduma za Afya za
Hospitali, na Wananchi wote kwa ujumla katika kuwasimamia, kuwaelekeza
na kutambua mapungufu ya kimfumo au yale yanayohusu watumishi wa afya
yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili mara moja. Ni lazima tuzingatie
Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutimiza jukumu hili. Wizara ya Afya
itaendelea kuvijengea uwezo Mabaraza ya kitaaluma ya wataalamu wa afya
ili kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Tufanye kazi kwa pamoja ili kutekeleza kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, inayosema ‘HAPA KAZI TU’.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mtwara – Tanzania
29 Machi 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni