WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Kamati ya Uchumi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi ikutane na wafanyabiashara wote ili wajadiliane na
kupanga kiwango cha ushuru kinachopaswa kutozwa kwenye mazao ya wilaya
hiyo.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 3, 2016) wakati akizungumza
na mamia ya wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye uwanja wa michezo wa Dutwa, Wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.
Amefikia
uamuzi huo baada ya kuona bango lililoshikwa na wananchi wakilalamikia
kutozwa ushuru wa sh. 3,000/- kwa gunia moja la mazao badala ya sh.
1,000/- ya zamani.
"Masuala
ya ushuru ni maamuzi baina yenu na Halmashauri yenu lakini hiyo tozo
imeongezwa sana kutoka sh. 1,000/- hadi sh. 3,000/-. Ninaiagiza Kamati
ya Ucumi ikae na wafanyabiashara wote ili mjadili suala hili na
mkubaliane kiwango cha ushuru."
"Wabunge
pia waalikwe kwenye kikao hicho na Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na
Baraza la Madiwani nalo pia lishiriki kikao hicho. Kama mnataka
kupandisha ushuru ni lazima mkubaliane viwango ili Watanzania wafanye
biashara wakiwa na mapenzi na nchi yao," alisema huku akishangiliwa.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alifafanua kwamba suala la kulipa ushuru ni la muhimu
katika kuchangia makusanyo ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
"Ushuru ni lazima ulipwe lakini pia ni lazima muwe mmekubaliana ni
kiwango gani mnatoza. Makusanyo yote haya tunayofuatilia kwa sasa ni
matokeo ya watu kulipa kodi na ushuru kama huu," alisisitiza.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amekataza tabia ya maafisa wa kutoza ushuru kudai
fedha kabla mwananchi hajauza mifugo wanapoileta mnadani kwani anakuwa
amekuja kutafuta fedha.
Alikuwa
akijibu hoja iliyotolewa na mbunge wa viti maalum (CHADEMA), Bi. Gimbi
Masabo ambaye alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna tabia ya kutoza sh.
6,000/- kwa kichwa kwa kila ng'ombe anayeswagwa kuingia eneo la mnada
bila kujali kama mtu huyo ameuza ng'ombe au hajauza.
"Hivi
unawezaje kumtoza mtu ushuru wakati hajauza chochote au wakati akiwa
njiani kuelekea mnadani? Ni bora umtoze mtu baada ya kuuza. Kumbukeni
kuwa wananchi wetu wanakuja mnadani ili wauze na kupata fedha ya kurudi
nayo nyumbani, sasa nyie mnamtoza kabla hajauza chochote au hata kama
hajauza. Acheni hiyo tabia," alisema.
Alimtaka
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Robert Lweyo aimarishe usimamizi wa
minada na kujua idadi ya mifugo ambayo inaingizwa, inayouzwa na ile
inayobaki ambayo imeshindikana kuuzwa.
"Jipange
wewe Mwenyekiti na timu yako ya watoza ushuru mfuatilie agizo hili.
Mkiwa wavivu ndiyo mnakuja na maamuzi haya ya jumla jumla ya kuanza
kutoza ushuru hata mtu akiwa njiani anakuja mnadani kutafuta fedha,"
alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akitoa
taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Bw. Ponsiano Nyami
alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ofisi kwa
sababu majengo ya iliyokuwa ofisi ya wilaya hivi sasa yanatumiwa na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hali iliyowalazimu wahamie kwenye ofisi za
Halmashauri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 3, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni