Chama cha
Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimemfukuza uanachama Mwanasiasa Mkongwe
Hassan Nassor Moyo baada ya kubainika amekuwa akifanya vitendo
vinavyokwenda kinyume na maadili ya chama ikiwamo kuhutubia mikutano ya
hadhara inayoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) na kukejeli misingi ya
Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imefahamika visiwani
humo jana.
Uamuzi wa
kumfukuza mwanasiasa huyo ulifikiwa jana na Kikao cha Halimashauri Kuu
ya CCM Mkoa wa Magharibi kilichofanyika katika Tawi la CCM Mbweni chini
ya Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Yussuf Mohamed Yussuf ambapo wajumbe wote
waliunga mkono ajenda ya moyo kufukuzwa uanachama wake.
Akizungumza
na waandishi wa habari Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Azziza Mapuri alisema
kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao kujiridhisha kuwa Mzee Moyo
alikuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyume na miiko na maadili ya
chama.
Mapuri
alisema kwamba uchunguzi uliyofanywa kuanzia ngazi ya Tawi Fuoni, Jimbo,
Wilaya hadi Mkoa ripoti zote zimeonyesha Moyo alikuwa akivunja miiko na
maadili ya chama kutokana na kitendo chake cha kuhudhuria mikutano ya
CUF na kupanda katika majukwaa na kukejeli misingi ya mapinduzi na
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Kwa
kutumia Ibara ya 93 (14) ya Katiba ya CCM Mzee Moyo tumemfukuza
uanachama wa CCM baada ya kikao kupitia ripoti zote za uchunguzi na
kujiridhisha alikuwa akivunja maadili na miiko ya chama chake," alisema
Mapuri.
Alisema
kwamba katiba ya CCM imeweka miongozo, maadili na kanuni na kila
mwanachama wake anatakiwa kuheshimu, lakini Mzee Moyo ameshindwa
kuheshimu na kufikia kukosoa chama hadharani badala ya kutumia taratibu
za vikao vya chama.
Alisema
kutokana na nguvu za kikatiba walizopewa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya
mkoa kupitia kifungu cha 93 (14) cha katiba ya CCM, Mzee Moyo amefukuzwa
bila ya kuhitaji baraka za wazee wa chama kwa vile ni utekelezaji wa
katiba.
Hata
hivyo alisema kwamba kama Mzee Moyo atakuwa hakuridhika na uamuzi huo
bado ana haki ya kukata rufaa katika vikao vya ngazi ya juu, lakini
alisema kulingana na ushaidi waliokusanya Moyo hawezi kushinda sehemu
yoyote hata kama akiamua kukimbilia mahakamani.
Akizungumza
na Mwananchi jana Moyo alisema kwamba ameshangazwa na uamuzi huo, hata
hivyo hafikirii kukata rufaa kwa sababu haoni sababu za msingi za
kuendelea kubakia ndani ya CCM wakati wameonyesha hawamtaki.
Moyo
alisema kwamba yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ndiyo maana
amekuwa akifanya kazi ya kulinda misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa
(SUK) kwa kuwakumbusha viongozi na wananchi umuhimu wa kuwepo kwa
serikali ya pamoja kupitia mikutano ya hadhara na makongamano.
"Sina
mpango wa kukata rufaa sioni umuhimu wa kubakia CCM kama wenyewe
hawanitaki na wala sina nia ya kukata rufaa, " alisema Moyo.
Hata
hivyo alisema yupo safarini nje ya Zanzibar lakini hadi jana alikuwa
bado hajapokea rasmi barua ya kufukuzwa uanachama wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni